UHURU FM
Moto mkubwa wasababisha maafa California, Marekani

MAENEO ya jimbo la California ambayo hukuza mizabibu yameathiriwa na moto mkubwa ambao unaenea kwa kasi sana na kusababisha vifo vya watu 10.

Mamia ya watu wamehamishwa makwao na inakadiriwa kwamba zaidi ya nyumba 1,500 zimeharibiwa na moto huo.

Watu saba waliuawa katika wilaya ya Sonoma, maafisa wamesema.

Watu zaidi ya 20,000 wamekimbia wilaya za Napa, Sonoma na Yuba baada ya moto mbaya zaidi wa nyika kuzuka maeneo hayo.

Gavana wa jimbo la California ametangaza hali ya dharura.

"Moto huu umeharibu sana nyumba na miundo mbinu mingine na unaendelea kutishia maelfu ya nyumba, jambo ambalo limesababisha haja ya kuwahamisha maelfu ya watu," taarifa ya gavana imesema.

Kando na watu waliofariki Sonoma, wengine wawili wamefariki Napa na mwingine mmoja Mendocino.

Inaarifiwa kwamba kuna majeruhi wengine zaidi na wapo pia watu ambao bado hawajulikani waliko.

Marian Williams mkazi wa Kenwood, Sonoma amesema yeye na majirani zake waliutoroka moto huo kwa msafara wa magari.

"Ni moto mkubwa ajabu, hatujawahi kuona moto kama huo," ameambia shirika la utangazaji la NBC.

Mkuu wa idara ya misitu na kinga dhidi ya moto California Kim Pimlott, amesema nyumba 1,500 kufikia sasa zimeharibiwa.

Chanzo cha moto huo uliozuka Jumapili usiku bado hakijabainika.

Mkuu wa kukabiliana na moto wilaya ya Napa amesema hali ya kiangazi katika eneo hilo inaathiri juhudi za kuukabili moto huo na kwamba wameomba usaidizi kutoka wilaya nyingine jirani.

Wafanyakazi wengi wa mashamba hayo ya mizabibu wamehamishiwa maeneo salama kwa ndege.

Moto huo unaenea kwa kasi sana kutokana na upepo mkali, ukavu na joto kali.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imetoa tahadhari eneo lote la San Francisco na kusema "moto ukizuka basi kuna uwezekano utaenea kwa kasi sana".

Mmiliki mmoja wa mizabibu aliambia gazeti la LA Times kwamba anaamini shamba lake limeharibiwa baada yake na familia yake kukimbilia usalama Jumapili.

"Upepo ulikuwa unazuka na kufifia. Ndimi za moto zilituzingira," amesema Ken Moholt-Siebert.

Maafisa wa kuzima moto California wanakadiria kwamba eka 70,000 zimeteketezwa na moto huo.

Jimbo la California limekuwa likiathiriwa na moto miezi ya karibuni.

Septemba moto mkubwa uliathiri jiji la Los Angeles.

Source: BBC

RECENTS
MICHEZO
Leo Jumanne Januari 16, 2018 klabu ya Yanga imeingia mkataba wa miaka mitatu (3) na kampuni ya utengenezaji wa vifaa vya michezo ya Macron ambayo makao makuu yake yapo nchini Italy, Macron watakuwa ndio watengenezaji wakuu wa vifaa vyote michezo vya klabu hiyo.
January 16, 2018
Read More
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF imewapeleka kwenye kamati ya Maadili viongozi wanne kwa kughushi na udanganyifu.
January 16, 2018
Read More
HABARI ZA JUU
KITAIFA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 15 Februari, 2018 amemuapisha Luteni Jenerali Yacoub Hassan Mohamed kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
February 15, 2018
Read More
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, imesema Mvua za Wastani Mpaka juu ya Wastani zinatarajiwa kuanza kunyesha katika kipindi cha wiki ya Kwanza ya Mwezi Machi hadi Mei mwaka huu katika maeneo mengi hapa nchini.
February 15, 2018
Read More
Serikali imesema imekamilisha uhakiki wa madai ya Watumishi wa Umma na kwamba kiasi cha shilingi Bilioni-43.39 ambacho ni madai halali kitalipwa kwa mkupuo pamoja na mshahara wa mwezi Februari mwaka huu.
February 09, 2018
Read More
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imesema katika kipindi cha Mwezi Januari hadi Disemba mwaka jana, jumla ya Askari Polisi Mia Moja na Tano waliotenda makosa mbalimbali, walichukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.
February 09, 2018
Read More