UHURU FM
Kiongozi wa mikakati wa upinzani Kenya David Ndii akamatwa

MMOJA wa wakuu wa mikakati wa muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (Nasa) anazuiliwa na polisi siku chache baada ya kuteuliwa kuongoza moja ya makundi ya muungano huo.

Bw David Ndii, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, alikuwa ameteuliwa kuongoza Kamati ya Taifa ya kusimamia Mabunge ya Wananchi.

Mabunge hayo ya wananchi yaliundwa na Nasa, chini ya waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, kama njia ya kushinikiza mageuzi nchini humo baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ambao Bw Odinga na muungano wake walisusia.

Bw Ndii alikamatwa Jumapili jioni akiwa kwenye hoteli moja jimbo la Kwale pwani ya Kenya.

Mkewe, Mwende Gatabaki, akiwahutubia wanahabari, amesema mumewe alikamatwa na wanaume saba ambao walimfahamisha kwamba angepelekwa kito cha polisi cha Diani lakini walipofika huko hawakumpata.

"Walikuwa wanatudanganya, kama watoto," amesema.

Kadhalika, walitaka kuingia kwenye chumba chao hotelini kufanya ukaguzi lakini alipowauliza kibali cha kufanya upekuzi wakasema hawakuhitaji kibali hicho kwa sababu walikuwa wakuu wa kituo cha polisi.

Aidha, walikuwa wanatafuta kompyuta ambazo Bi Gatabaki anasema hawakuwa nazo chumbani.

Amesema polisi hawakueleza sababu ya kukamatwa kwake na kwamba alipozidi kuuliza maswali kuhusu alipokuwa mumewe naye alikamatwa na kuzuiliwa kwa muda.

Bi Gatabaki amesema familia hiyo ilikuwa likizoni Kwale na pia kwa ajili ya kuhudhuria harusi ya mpwa wao.

Upinzani umeshutumu hatua ya polisi na kuwataka kumwachilia huru Bw Ndii.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, ambaye ni mwanachama wa muungano wa Nasa, amesema polisi wamewafahamisha kwamba mwanamikakati huyo atashtakiwa kwa tuhuma za uchochezi.

"Mashtaka hayo yanahusiana na maneno aliyoyatamka miezi mingi iliyopita. Kawaida, walifaa kumuita kwa mahojiano na si kumvamia akiwa likizoni," amenukuliwa na kituo cha habari cha NTV.

Bw Ndii ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Jubilee yake Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto na huandika makala yanayochapishwa mwishoni mwa wiki katika moja ya magazeti makuu nchini humo.

Alizua utata alipopendekeza kwamba baadhi ya majimbo Kenya yanaweza kujitenga iwapo mabadiliko hayatafanikiwa katika siasa na uongozi nchini Kenya.

Muungano wa upinzani uliunda kundi la watu sita kuongoza Mabunge ya Wananchi huku ukiendelea na juhudi za kushinikiza mageuzi nchini humo.

Bw Odinga alisema Mabunge ya Wananchi yatajumuisha wadau kutoka nyanja mbalimbali na yatatumiwa kutoa mwelekeo kwa nchi.

Wiki iliyopita, alidokeza kwamba mabunge hayo yatashirikishwa katika mpango wake wa kutaka kuapishwa kuwa kiongozi wa Kenya tarehe 12 Desemba.

Majimbo kumi kati ya 47 nchini Kenya, ambayo yana viongozi na wafuasi wengi wa upinzani, tayari yamepitisha hoja ya kuundwa kwa mabunge hayo.

Source: BBC

RECENTS
MICHEZO
Leo Jumanne Januari 16, 2018 klabu ya Yanga imeingia mkataba wa miaka mitatu (3) na kampuni ya utengenezaji wa vifaa vya michezo ya Macron ambayo makao makuu yake yapo nchini Italy, Macron watakuwa ndio watengenezaji wakuu wa vifaa vyote michezo vya klabu hiyo.
January 16, 2018
Read More
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF imewapeleka kwenye kamati ya Maadili viongozi wanne kwa kughushi na udanganyifu.
January 16, 2018
Read More
HABARI ZA JUU
KITAIFA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 15 Februari, 2018 amemuapisha Luteni Jenerali Yacoub Hassan Mohamed kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
February 15, 2018
Read More
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, imesema Mvua za Wastani Mpaka juu ya Wastani zinatarajiwa kuanza kunyesha katika kipindi cha wiki ya Kwanza ya Mwezi Machi hadi Mei mwaka huu katika maeneo mengi hapa nchini.
February 15, 2018
Read More
Serikali imesema imekamilisha uhakiki wa madai ya Watumishi wa Umma na kwamba kiasi cha shilingi Bilioni-43.39 ambacho ni madai halali kitalipwa kwa mkupuo pamoja na mshahara wa mwezi Februari mwaka huu.
February 09, 2018
Read More
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imesema katika kipindi cha Mwezi Januari hadi Disemba mwaka jana, jumla ya Askari Polisi Mia Moja na Tano waliotenda makosa mbalimbali, walichukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.
February 09, 2018
Read More