UHURU FM
Naibu Waziri Nishati aagiza utekelezaji REA III uanze haraka
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akionyesha kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wa Kata ya Ibanda (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Wilayani Kyela. Kifaa hicho hutumiwa na wananchi wenye nyumba ya vyumba vichache ambao hawahitaji kufanya wiring.

SERIKALI imeagiza utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) uanze mwezi huu wa Januari, 2018 sambamba na utekelezaji wa Mradi wa Densification ambao upo kwenye utekelezaji.

Naibu Waziri Nishati, Subira Mgalu ametoa agizo hilo Januari 6, 2018 wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo mbalimbali ambayo Mradi wa Umeme Vijijini unatekelezwa Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya.

Mgalu alizungumza na baadhi ya wananchi Wilayani humo ambao walimueleza kero mbalimbali zinazohusu masuala ya Nishati ya Umeme ambayo ni kukatika kwa umeme mara kwa mara bila taarifa, kucheleweshwa kuunganishwa na huduma ya umeme kwa ambao tayari wamelipia, baadhi ya Taasisi (shule, zahanati, vituo vya afya na visima vya maji) kurukwa wakati wa utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II).

Baada ya kuzungumza na wananchi hao kwa nyakati tofauti, akijibu kero zao, Naibu Waziri Mgalu aliagiza Mradi wa REA III uanze kutekelezwa ndani ya Mwezi huu wa januari, 2018 bila kuchelewa. “Utekelezaji wa Mradi wa Densification ambao unafanyika hivi sasa, uende sambamba na utekelezaji wa Mradi wa REA III kuanzia Mwezi huu wa Januari, 2018,” aliagiza Mgalu.

Akizungumzia suala la kucheleweshwa kuunganishwa na huduma ya umeme kwa wananchi waliolipia, Mgalu aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wateja wote waliolipia umeme wanaunganishwa mara moja bila kuwepo visingizio. “Tulikwisha agiza maombi yote ya wateja kuunganishiwa umeme yatekelezwe ndani ya Siku Saba baada ya kulipia,” alisema Naibu Waziri Mgalu.

Aidha, kuhusu suala la baadhi ya maeneo kurukwa hususan maeneo ya huduma za kijamii zikiwemo shule, zahanati, vituo vya afya na visima vya maji, Naibu Waziri Mgalu alisisitiza kwamba wakati wa utekelezaji wa Mradi huo wa REA III, maeneo hayo yapewe kipaumbele.

“Tunakiri utekelezaji wa REA II, ulikuwa na mapungufu ikiwemo ya kuruka baadhi ya maeneo, ninawahakikishia kasoro hii haitojirudia kwenye REA III,” alisema.

Aliongeza kuwa TANESCO itoe taarifa mapema kwa Wananchi kama kutakuwa na ukataji wa umeme kutokana na sababu mbalimbali na kwamba iongeze ubunifu katika utekelezaji wa shughuli zake ikiwemo kuwafuata wateja na kufungua Vituo maeneo ya Vijijini ili kuwarahisishia wananchi wa maeneo hayo upatikanaji wa huduma.

Aidha, baadhi ya maeneo ulikopita Mradi wa Umeme Vijijini wa REA aliyotembelea Naibu Waziri Mgalu katika ziara hiyo Wilayani Kyela ni Bandari ya Itungi; Kata ya Kajunjumele; Kata ya Nkuyu; Kata ya Ibanda na Kata ya Kasumulu.

Bandari ya Itungi ni mnufaika wa Mradi wa REA II ambapo baadhi ya shughuli zake hutekelezwa kwa kutumia Nishati ya Umeme ikiwemo shughuli inayoendelea hivi sasa ya Uundaji wa Meli ya abiria inayofanywa na Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd.

Naibu Waziri Mgalu yupo Mkoani Mbeya kwa ajili ya ziara ya kukagua utekelezaji  Miradi ya Umeme Vijijini na Miradi mingine ya umeme Mkoani humo.

RECENTS
MICHEZO
Kimbembe cha Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kinaendelea leo Jumamosi (Januari 13, 2018) kwa mechi nane za raundi ya 13 kupigwa katika viwanja nane tofauti.
January 13, 2018
Read More
KOREA Kaskazini imesema kuwa itatuma ujumbe wake katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi 2018 inayotarajiwa kufanyika Korea Kusini mnamo mwezi Februari kulingana na mji wa Seoul.
January 09, 2018
Read More
HABARI ZA JUU
KITAIFA
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewasihi wananchi wa Tanzania kuendelea kuwaombea Dua na visomo mbali mbali Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wanaouawa wakilinda Amani katika nchini mbali mbali ikiwemo DRC Kongo.
January 22, 2018
Read More
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema wizara yake haina mpango wa kuongeza tena muda zoezi la utambuzi wa mifugo na kuwataka wafugaji popote walipo nchini kupaza sauti zao ili kuhakikisha kuwa ng’ombe na punda wote wamepigwa chapa ifikapo Januari 31 mwaka huu.
January 20, 2018
Read More
ZOEZI la ugawaji wa Miguu ya kisasa ya bandia kwa watu wenye ulemavu wa Miguu awamu ya pili limeanza jana, ikiwa ni Kampeni iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda ya kuwapatia Miguu ya kisasa inayowawezesha kufanya shughuli za uzalishaji Mali Kama awali ambapo imejidhihirisha kuwa RC Makonda akiahidi jambo analitimiza kwa vitendo na sio Siasa.
January 20, 2018
Read More
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar Balozi Ali Abeid Karume kusitisha usajili wa meli mpya hapa nchini mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.
January 19, 2018
Read More